KILIMANJARO MARATHONI 2014 YAWATEGA WAANDISHI WA HABARI.
![]() |
| Dk Fenella Mukangara |
Waziri
wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dk. Fenella Mukangara anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi kwenye mbio mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon ambazo zinatarajiwa
kufanyika Jumapili ijayo tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.
Aggrey
Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo alisema
jana kwamba Dr. Mukangara amekubali kuwa mgeni rasmi na atahuduria sherehe ya
utoaji zawadi ambapo atatoa zawadi kwa washindi kumi wa mbio defu za kilomita
42 maarufu kama Full Marathon kwa wanaume na wanawake.
“Uwepo
wa waziri ni ishara ya uungaji mkono tukio hili na ameeleza kufurahishwa kwake
na maandalizi ya hali ya juu ya Kilimanjaro Marathon. Dk. Mukangara ameeleza
mara kadhaa kwamba serikali inaunga mkono Kilimanjaro Marathon kwa kutambua
mchango wake michezo, utalii na uchumi,” alisema Marealle.
Marealle
aliongeza kwamba baada ya sherehe ya utoaji zawadi Waziri ataungana na Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro na mpenda michezo Mhe. Leonidas Gama, wawakilishi wa
wadhamini na watu wengine mashuhuri kwenye mlo maalum wa mchana
uliodhaminiwa na Kibo Palace Hotel.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro binafsi na kupitia ofisi yake amekuwa muungaji mkono wa
Kilimanjaro Marathon na amekuwa akifurahia kukaribisha maelfu ya watu wanaokuja
Moshi kutoka mataifa mbalimbali.
Kutangazwa
kwa Dk Mkangara kuwa mgeni rasmi ni kama mtego kwa waandishi wa habari za
michezo kutokana na kuwepo kwa msimamo wa kutotangaza wala kuandika
habari zinazomhusu Waziri huyo pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari(Maelezo), Assah Mwambene kama sehemu ya kupinga mwenendo wa serikali wa
kuvifungia vyombo vya habari.
Msimamo
huo ulitolewa Oktoba mwaka jana na wadau
na taasisi mbalimbali za habari ambapo katika taarifa yao walisema pia
wamesikitishwa na tabia iliyoonyeshwa na Dk Mukangara na Mwambene kuchukua
uamuzi wa kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania bila kuyasikiliza na
kupotosha umma juu ya jambo hilo.
Katika
hatua nyingine Mkurugenzi
Mkuu wa Wild Frontiers ambao ndio waandaaji wa mbio hizo John Addison alisema
“mbio za mwaka huu zimesheheeni motisha mbalimbali za kuvutia ili kuongeza
idadi ya washiriki.
Washindi
wa kwanza kwenye mbio ndefu za kilomita 42 (Kilimanjaro Premium Lager Marathon)
wanawake kwa wanaume watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 4 kila mmoja,
shilingi milioni mbili kwa washindi wa pili na shilingi milioni 1 kwa washindi
wa tatu.
Washindi
wa kwanza kwenye mbio ndefu za nusu marathon (km 21) wanawake kwa wanaume
watajinyakulia kiasi cha shilingi milioni 2 kila mmoja, shilingi milioni 1 kwa
washindi wa pili na shilingi 500,000 kwa washindi wa tatu.
Addison
aliongeza kuwa medali na t-shirt zitatolewa kwa wanariadha 500 wa kwanza
kumaliza mbio za kilomita 42, wanariadha 2,200 wa kwanza kumaliza mbio za nusu
marathon na wanariadha 80 wa kwanza kumaliza mbio za walemavu. Washiriki
3,000 wa kwanza kumaliza mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run watapewa
t-shirts baada ya kumaliza mbio na watapata fursa ya kujishindia zawadi
mbalimbali za kuvutia kupitia droo.

Comments
Post a Comment