MSHITAKIWA KESI YA KUSAFIRISHA TWIGA AUGUA GHAFLA

Moshi

MAHAKAMA ya hakimu mkazi mjini Moshi jana imelazimika kuahirisha kesi ya utoroshwaji wa Twiga kwenda Uarabuni baada ya mshtakiwa wa kwanza
katika kesi hiyo Kamran Ahmed,kuugua ghafla muda mchache kabla ya kufika mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa wakili wa mshtakiwa huyo Edmund Ngemela aliieleza mahakama hiyo kwamba mshtakiwa huyo Sukari imepanda na hivyo kushindwa kufika mahakamani kuendelea na kesi inayomkabili.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Simoni Kobelo na mawakili wa pande zote mbili, Ngemela alisema kulingana na hali ya afya ya mteja wake ilikuwa ni vigumu kufika mahakamani hapo.

"Mheshimiwa hakimu kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuendelea na mashahidi upande wa mashtaka,lakini niiombe mahakama yako tukufu, kuaihirisha kwani mteja wangu, sukari imepanda kuliko kiwango cha
kawaida"alisema

Katika kesi hiyo iliyolazimika kuzungumzwa katika mahakama ya ndani(Chamber court) upande wa mawakili wa serikali haukuwa na pingamizi na maombi hayo na kutaka mahakama kufuata taratibu zake.

Kesi hiyo ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi ambapo upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili Evetha Mushi, Joseph Maugo na Steven Mwanasenjele ilifika kwa ajili ya kuongoza mashahidi wao kuendelea na ushahidi katika kesi hiyo.

Tayari upande wa mashtaka umeleta jumla ya mashahidi 21 na kwamba Februari 26 ilikua ni mwendelezo wa mashahidi wake kufika mahakamani hapo.

Kufuatia maombi hayo,hakimu Kobelo aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 21, 24 na 25 mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama,wakili Ngemela alisema mteja wake alimuacha nyumbani kwake asubuhi akiwa katika mipango ya kwenda hospitali kwa ajili ya kutazama Zaidi afya yake.

Hata hivyo kesi hiyo ambayo ilipangwa kusikilizwa kuanzia saa 3.00 asubuhi katika mahakama ya wazi,lakini wanahabari walijikuta wakisubiri hadi saa 4.55 asubuhi bila kufahamu kilichoendelea hadi walipotaarifiwa kesi inaahirishwa katika mahakama ya ndani.

Juzi shahidi wa 20,Robert Nyanda alielezea mazingira ya siku ya tukio na alivyopokea maelekezo kutoka kwa bosi wake Rosemary Isarael ya kuandaa vifaa vya kuinua vitu vizito kwa ajili ya kupakia wanyama hao
katika ndege ya Qatar.

Aidha shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa siku ya tukio wanyama hao walipakiwa katika ndege hiyo majira ya saa nane usiku huku wakiletwa uwanjani hapo na gari aina ya Fuso pamoja na vijana maalum
kwa ajili ya kusaidia upakiaji wake katika ndege.

Naye shahidi wa 21, Rewald Amani alieleza mahakama kuwa ndege hiyo ilitua nchini Novemba 24 na kuondoka Novemba 26 mwaka 2010 ikiwa salama bila kuwapo kwa tatizo lolote.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na raia wa Pakistan, Kamran Ahmed, Hawa Mang'unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.

Comments

Popular posts from this blog

MGOMO WA WAFANYABIASHARA WATIKISA MKOANI KILIMANJARO.

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO,SAID MECKY SADICKY AFANYA ZIARA KATIKA MAGHALA NA MADUKA YA MARENGA INVESTMENT KUJIONEA HALI YA TATIZO LA SUKARI

MREMA AENDELEA NA MIKUTANO JIMBONI KWAKE VUNJO