MTUHUMIWA MMOJA KESI YA MAUAJI YA BILIONEA WA MADINI AACHIWA HURU.



Na Mwandishi wetu.

OFISI ya mkurugenzi wa Mashtaka Nchini imemfutia mashtaka ya mauaji,mmoja  kati ya watuhumiwa nane wa mauaji ya kukusudia dhidi ya
mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite bilionea , Erasto Msuya (43).

Hati ambayo imetumika kumwachia huru Joseph Damas (Chusa) ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wa madini hayo  imetolewa na kusainiwa na
mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Elieza Feleshi na kisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuiwasilisha kwa Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Munga Sabuni .

Hati hiyo ambayo hufahamika kama “Nolle Prosecution “ilitolewa mbele ya mahakama hiyo April 16 mwaka huu kwa ajili ya kuingiza rasmi katika kumbukumbu za Mahakama.

 “Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii, umekamilika na ikikupendeza, upande wa mashitaka tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi kabla ya kulipeleka jalada lenye mashitaka haya, Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya kukusudia namba 06 ya mwaka 2013.”alieleza Julius Semali wakili wa serikali.

“Tumepokea hati ya kuachiwa huru kwa mshitakiwa namba 07, Joseph Damas,”alisema Wakili  Semali.

Baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, Hakimu Munga aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 06 mwaka huu na kuamuru washitakiwa saba, waliosalia katika kesi hiyo kurejea rumande hadi hapo, shauri hilo litakapotajwa
tena mahakamani hapo ikiwa ni kwa ajili ya kusoma maelezo ya mashahidi.

Bilionea Msuya aliuawa mwezi Agosti mwaka jana kwa kupigwa, majira ya saa 6:30 mchana kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, eneo la Mijohoroni, Wilaya ya Hai, Karibu na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kufa papo hapo.

Washitakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia ni Sharif Mohamed Athuman (31), Mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredii (38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.

Wengine ni Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir a.k.a “Msudani” au “Mnubi”(32), mkazi wa Dar es salaam na Lang’ata Wilayani Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Kijiji cha
Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa Majeshi, mkazi wa Babati mkoa wa Manyara.

Comments

Popular posts from this blog

MGOMO WA WAFANYABIASHARA WATIKISA MKOANI KILIMANJARO.

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO,SAID MECKY SADICKY AFANYA ZIARA KATIKA MAGHALA NA MADUKA YA MARENGA INVESTMENT KUJIONEA HALI YA TATIZO LA SUKARI

MREMA AENDELEA NA MIKUTANO JIMBONI KWAKE VUNJO