WIZARA YA MALIASILI, ARDHI NA TAMISEMI KUMALIZA MGOGORO WA MPAKA WA HIFADHI YA NORTH UGALA NA VIJIJI JIRANI
NA HAMZA TEMBA- WMU- URAMBO, TABORA
...................................................................................
Naibu Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Wizara yake itashirikiana na Wizara ya
TAMISEMI na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa
uamuzi wa pamoja wa kumaliza mgogoro wa mpaka baina ya Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na
vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja wilayani Urambo .
Naibu Waziri Hasunga amesema
hayo mkoani Tabora jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani
humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Akiwa mkoani humo alitembelea
eneo lenye mgogoro, akafanya mkutano wa hadhara na wananchi na viongozi
mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kutafuta majibu ya kutatua mgogoro huo.
Akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme, Mkazi wa Kijiji
hicho, Ramadhan Rashid alisema wananchi wa vijiji hivyo wanailalamika Serikali
kupitia Wakala wa Huduma za Misitu kwa kusogeza mpaka wa hifadhi hiyo hadi
ndani ya ardhi ya vijiji wakati wa uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka. Alisema
eneo hilo ni la vijiji hivyo tangu mwaka 1988.
Naye, Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa Wakala
wa Huduma za Misitu Tanzania, Peter Maiga alisema hifadhi hiyo
ilianzishwa mwaka 1956 ikiwa na hekta 165,282 huku mipaka yake halisi ikiwa
haijabadilishwa. Alisema zoezi la uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka lilizingatia
mipaka halisi kwa kutumia mfumo wa GPS.
Kwa upande wake Mbunge
wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji
hivyo kwenye mkutano huo, alisema idadi ya wananchi inaongezeka huku maeneo yakiwa
hayaongezeki hivyo akaiomba Serikali ione uwezekano wa kuwaongezea wananchi
maeneo ya kulima na kuendeshea maisha yao.
Akijibu malalamiko na
maombi ya wananchi hao wa Urambo, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya
awamu ya tano imedhamiria kutatua kero za wananchi sambamba na kuwaletea
maendeleo.
“Baada ya kukagua eneo
hili na kusikiliza pande zote, tunaenda kukaa pamoja na Wizara ya TAMISEMI na Wizara
ya Ardhi tuangalie ramani zote zilizopo, Matangazo ya Serikali (GN) na taarifa
mbalimbali ili tujiridhishe ni ipi mipaka halali tufikie ufumbuzi wa mwisho,
migogoro ya namna hii haiwezi kuisha bila kushirikisha wizara hizi.
“Nawaagiza watendaji
wangu kwenye taasisi mshirikiane na wananchi muwaelimishe na mzuie wasiendelee
na uharibifu hadi hapo tutakapopata suluhu ya mgogoro huu”. alisema Naibu Waziri Hasunga.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri huyo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujiepusha na vitendo
vya kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. “Mkiingiza mifugo tukaikuta
tutaitaifisha kwa mujibu wa sheria” alisema Naibu Waziri Hasunga.
Aidha aliwataka
wananchi hao kujikita kwenye shughuli za ufugaji nyuki kibiashara kwa kutumia
mizinga ya kisasa ambayo huongeza uzalishaji. “Asali ina soko zuri duniani kwa
sasa, bei yake ni nzuri, kila mtu afuge tuchangie uchumi wa taifa letu” alisema
Hasunga.
Naibu Waziri Hasunga ataendelea
na ziara yake ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi katika mikoa wa Katavi, Rukwa na
Songwe.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Kangeme kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu
wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora
jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili
kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati)
akisikiliza maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kushoto) kuhusu
mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme,
Utenge na Mtakuja baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha
Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara
ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati)
akiteta jambo Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kulia) na Mwenyekiti wa
CCM wilaya ya Urambo, Mussa Mohammed (kushoto) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi
ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja baada
ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo
mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi
kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa
pili kushoto) akikagua ramani ya eneo lenye mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North
Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja alipokagua eneo hilo
katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara
yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa
kumaliza mgogoro huo.
Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza katika mkutano huo.
Mmoja ya wananchi akitoa kero yake katika mkutano huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kangeme
wakimpongeza kwa kumpigia makofi, Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko
pichani) baada ya kutoa ahadi ya kutatua mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu
wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja kwa kushirikisha
Wizara ya TAMISEMI na Ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji
cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana.
Mkutano ukiwa unaendelea.
Comments
Post a Comment