DK. KIGWANGALLA AFUNGA MAFUNZO YA 15 YA JESHI USU KWA MAAFISA WANYAMAPORI WA TAWA, TANAPA NA NGORONGORO MKOANI KATAVI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akiwaongoza Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kupiga gwaride la ukakamavu muda mfupi baada ya
kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele
mkoani Katavi.
Na Hamza Temba- Mlele, Katavi
...........................................................................
WAZIRI wa Maliasili na
Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza wahifadhi wote nchini kushirikiana na
wadau wengine hasa mamlaka za Mikoa na Wilaya katika maeneo yenye uvamizi wa
mifugo na migogoro ya mipaka ya hifadhi ili kutatua changamoto hizo kwa namna
shirikishi ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi
wanaozunguka maeneo hayo.
Ametoa agizo hilo jana
Disemba, 16, 2017 katika Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wakati akifunga mafunzo
ya 15 ya mabadiliko ya kuelekea mfumo wa Jeshi Usu kwa Maafisa wa Wanyamapori
87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za
Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
“Kazi ya ulinzi wa
rasilimali zetu za asili ni yetu na tutaiendeleza, Falsafa yetu ni
kuwashirikisha wadau wote, kama kuna taasisi za kiraia kwenye eneo lako la
kazi, taasisi za kijamii, mamlaka za mikoa na wilaya, wananchi, halmashauri
husika mshirikiane nao ili kupunguza madhara ya operesheni zetu, na zoezi hili
la uhifadhi liwe endelevu,” alisema Dk. Kigwangalla.
Aidha, alitoa wito kwa
wananchi wote kuendelea kuheshimu Sheria za nchi na kuacha kufanya shughuli za
kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo kuingiza mifugo, kuanzisha kilimo,
makazi na ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na matumizi mengineyo.
Awali akizungumzia
mafunzo hayo alisema, lengo ni kubadilisha utendaji katika sekta ya uhifadhi
kutoka ule wa kiraia kwenda wa jeshi usu ambao utaongeza nidhamu, uwajibikaji,
uadilifu na maadili kwa watumishi wote wa sekta hiyo ili waweze kusimamia
ipasavyo uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa.
Alisema katika
kuelekea mfumo huo, Jeshi hilo litakuwa moja bila kubagua taasisi yeyote ambayo
ipo chini ya Wizara yake. “Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 inampa
Waziri mamlaka ya kuunda Jeshi Usu, haikusema jeshi la TAWA, TFS, TANAPA au
NGORONGORO na kwa vile hili jeshi ni langu nataka liwe moja, na tunakimbiza
mchakato huu kwa haraka ukamilike kwa mujibu wa Sheria.
“Tunafarajika Mhe.
Rais ameshaunga mkono na ameshatupa maelekezo, Mwenyekiti wa Kamati ya Vyombo
vya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Ulinzi naye ameshasaini, ni
sisi sasa tuendelee kujipanga vizuri ndani ya wizara, tuanze kuishi kwenye
mfumo huo, kuanzia kwenye sare, uratibu wa mafunzo, uongozi na mfumo wa utawala,”
alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema mfumo huo wa
Jeshi Usu utakuwa na mnyororo mmoja wa mamlaka (chain of comand) na kwamba utahusisha
taasisi zote za uhifadhi zilizopo chini ya wizara yake kwenye sekta ya
wanyamapori, misitu na mali kale. “Sijawaona watu wa misitu hapa au mambo ya
kale, wote hawa ni ni muhimu, rasilimali za mali kale nazo ni muhimu sana
kulindwa kwani zikiharibika hazitengenezeki tena” alisema.
Katika hatua nyingine
amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa mafunzo yote ya Jeshi
Usu ambayo yanaendelea katika kituo cha Mlele, Mkoani Katavi yanaratibiwa moja
kwa moja na Wizara tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo uratibu unafanywa na
taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.
Akizungumzia mafanikio
ya vita dhidi ya ujangili na matunda ya mafunzo hayo alisema, “Katika siku za
hivi karibuni tumepiga hatua kubwa ya kupambana na ujangili hasa wa tembo, Kwa
dhati napongeza jitihada zinazofanywa na zinazoendelea kufanywa na wahifadhi,
maaskari watumishi wengine na wadau wetu wote kwa ujumla ambazo zimeimarisha
hali ya uhifadhi wa maliasili zetu”.
Alisema kwa kiasi
kikubwa matukio ya ujangili yamepungua na kwamba nyara nyingi zinazokamatwa katika
kipindi hiki ni za zamani ambazo zilikuwa zimefichwa na majangili kwa ajili ya
kuzitafutia masoko au kukimbia mikono ya sheria.
Alisema Wizara yake
itaendelea kutumia mbinu za kisasa za kiitelijensia za kukabiliana na ujangili
ikiwemo kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya doria na kuweka mifumo ya
kisasa ya mawasiliano ambayo haitaweza kuingiliwa na majangili au watu wengine
wenye nia ovu na uhifadhi.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Dk. Nebo Mwina akitoa nasaha
zake kwa wahitimu wa mafunzo hayo ya Jeshi Usu, aliwataka kuishi kwenye viapo
vyao kwa kudumu katika ukakamavu, uhifadhi, maadili mema na nidhamu.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Dk. James Wakibara
aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyopewa kufanya kazi kwa uaminifu na
uadilifu kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali, kujiepusha na
rushwa na kudhibiti vitendo vya ujangili.
Mhifadhi Gloria Bidebeli
kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA akisoma risala ya
wahitimu hao alisema mafunzo hayo yatawawezesha kuboresha ufanisi wa shughuli
za uhifadhi kwa kutii amri na kutekeleza maagizo kwa wakati.
Mafunzo hayo ya wiki
nne ambayo yalianza Novemba, 20 mwaka huu yalihusisha Mameneja wa Mapori ya
Akiba na Tengefu 20, Wakuu wa Kanda wa Kikosi Dhidi ya Ujangili wanane, Maafisa
Wanyamapori 29 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA,
Wahifadhi Wanyamapori watano kutoka TANAPA na Wahifadhi Wanyamapori 26 kutoka
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Mafunzo hayo
yalihusisha matumizi sahihi ya silaha, mbinu mbalimbali za kupambana na
uhalifu, huduma ya kwanza, ukakamavu, sheria mbalimbali zinazosimamia
maliasili, ukamataji na upekuzi wa wahalifu na jinsi ya kuwafungulia hati za
mashtaka.
Tangu kuanzishwa kwa
mafunzo hayo Septemba 2015 jumla wahifadhi 1468 wakiwemo Askari wa Wanyamapori
na Viongozi mbalimbali kutoka TAWA, TANAPA na NGORONGORO wameshapatiwa mafunzo
hayo katika kituo hicho cha Mlele.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla (wa pili kushoto) akikagua gwaride la Maafisa wa Wanyamapori 87 wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa
– TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro muda mfupi kabla ya
kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele
mkoani Katavi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akizungumza na Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu
mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara wakati wa hafla hiyo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja ya wahitimu wa mafunzo ya Jeshi
Usu kati ya Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya
Eneo la Ngorongoro jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa mafunzo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (katikati) akipokea salamu za Jeshi Usu wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akipokea salamu za Jeshi Usu wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo. Kulia ni Mkufunzi Mwandamizi wa Mafunzo hayo, Fidelis Kapalata.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla (wa pili kulia) akiangalia onesho la kulenga shabaha liliofanywa na
Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania–
TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi
Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya
ya Mlele, Rachel Kasanda na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania – TAWA, Dk. James Wakibara.
Maonesho ya klenga shabaha.
Maonesho ya klenga shabaha.
Maonesho ya klenga shabaha.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo.
Mhifadhi Gloria Bidebeli kutoka Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA akisoma risala ya wahitimu hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiaga baada ya hafla hiyo.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Comments
Post a Comment