Na Dixon Busagaga ,Ngorongoro.
MWANAMKE mmoja aliyepoteza Jicho,Masikio pamoja na Viganja
vya mikono yake miwili baada ya kushambuliwa na fisi wakati akinusuru mifugo
yake isiliwe katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ameiomba Serikali kumpatia
msaada ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kutoka katia eneo hilo.
Rose Kapande (50) Mkazi waa Kijiji cha Esapai kata ya
Nainokanoka wilaya ya Ngorongoro ,mkoani Arusha anasema alifikwa na mkasa huo
mwaka 2018 ,fisi huyo anayetajwa kuwa na
kichaa cha Mbwa pia akifanikiwa kuua Ng;ombe wanne .
Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro linatajwa kama
eneo la Uhifadhi Mseto ,masuala matatu yakifanyika kwa maana ya Uhifadhi
,uendelezaji wa jamii inayoishi katika eneo hili pamoja na utalii wakiruhusiwa
binadamu jamii ya wafugaji ,Mifugo ,Ng’ombe,Mbuzi na Kondoo kuishi pamoja na
Wanyamapori.
Hata hivyo utaratibu huo baadhi ya nyaraka zinaeleza
kuwa ulikuwa ni sehemu ya majaribio kuona kama inawezekana ukilenga kutizama
uwiano wa mambo matatu kwa maana ya Uhifadhi ,maendeleo ya jamii na utalii.
Changamoto iliyopo sasa kwa wakati huu ni idadi ya watu kuongezeka kutoka 8000
hadi kufikia 100,000 mara 10 zaidi,wakati hiofadhi hii ikianzishwa,mifugo
ikiongezeka hadi kufikia Milioni moja kutoka 260,000.
Ongezeko la idadi ya
watu na Wanyama limechangia kupungua kwa eneo la malisho pamoja na muingiliano
wa wanyamapori na wananchi ambao pia umechangia uwepo wa muingiliano wa
magonjwa yanayotoka kwa mifugo,wanyamapori na binadamu.
Matukio mbalimbali
ya vifo vitokanavyo na wanyapori kwa binadamu na wakati mwingine kusababisha
ulemavu yanatajwa kuchangiwa na ongezeko hili la Binadamu na mifugo .
Rose Kapande mama wa watoto
tisa aliyekuwa akiishi peke yake kwenye Boma baada ya kutalikiana na mumewe ni
mmoja wa waathirika wa matukio ya kuvamiwa na kisha kushambuliwa na Wanyamapori
,akipoteza viganja vya mikono ,Jicho moja ,Masikio pamoja na fuvu la kichwa .
Anaeleza kuwa wakati wa tukio, majira ya saa nane usiku
alikuwa amelala ndani peke yake siku
hiyo na baadae alisikia kitu kinagongagonga kwenye zizi la Ng’ombe ndipo
alipoamua kutoka nje kuona ni kitu gani .
Wakati anafungua mlango alimuona fisi akipambana na
mifugo yake upande wa Ndama ndipo kwa ujasiri alianza kumfukuza Fisi yule asile
mifugo ,wakati akimfukuza ghafla Fisi yule alimgeukia na kuanza kumshambulia
sehemu za mikono, kichwa na sehemu ya uso ambapo aliliwa jicho moja la upande wa kulia.
“Wakati natoka nje nikamwona fisi, nikawa namtishia ili aondoke, yule fisi
akanigeukia akaanza kupambana na mimi, alinishika na kuanza kunijeruhi kwa
kunichanachana sehemu ya fuvu la kichwa na sehemu ya uso upande wa kulia ambapo
alinitoa hadi jicho, kwa hiyo upande mmoja wote uliharibika na mikono yote
aliitafuna,”
“Baada ya kunijeruhi alirudi tena kwenye boma la Ng’ombe
na kuwajeruhi tena mifugo iliyokuwepo ndani, baada ya kuniachia nikiwa na
majeraha makali, nilipiga ukunga, bahati nzuri majirani zangu walikuja kunisaidia ambapo walinichukua na
kunipeleka hospitali ya KKKT, Karatu, baadaye nilipelekwa Hospitali ya Mount
Meru ambayo iko Arusha na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya
KCMC kwa matibabu makubwa zaidi,”alisema Rose .
Rose anasema kwa sasa hali ya maisha yake ni magumu kwa
kuwa hana mikono tena na upande mmoja wa kichwa na sehemu ya uso vyote
viliharibiwa na fisi na kwamba hawezi kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia
kipato.
“Mimi ni mlemavu, sina mikono na upande wangu mmoja wa
kichwa na uso ni mbovu, nipo tu hapa nasaidiwa na wasamaria wema maana watoto
wangu wote walishaolewa, kwa hiyo chakula nalishwa kama mtoto mdogo, nguo
navalishwa yaani sijiwezi chochote hapa nilipo,”alieleza Rose huku akisaidiwa
kunyweshwa uji.
“Naishukuru serikali nimepona mpaka kwa namna ambavyo walinipigania kuokoa maisha
yangu, nimebaki mlemavu na hali yangu ya Maisha ni ngumu, mpoaka sasa kutokana
na Maisha niliyopitia naishi kwa hofu hapa niluipo kutokana na Wanyama wakali
walipo katika hifadhi hii,”
Rose anasema kwa kuwa amekuwa akiishi kwa hofu ameiomba
serikali imsaidie aondoke katika eneo la hifadhi Ngorongoro imtafutie sehemu
nyingine ya kwenda kuishi kama ambavyo watu wanavyohamishwa kwa sasa.
“Mimi niliomba kuondoka hata kabla ya huu hili zoezi la
kuwaondoa watu halijaanza, naomba serikali inisaidie niende kuishi sehemu salama zaidi, nitafurahi sana maana
najua nitakwenda kuishi sehemu salama nikitoka huku hifadhini maana maisha
yangu kwasasa yamekuwa na hofu kubwa sana tangu nijeruhiwe,” alieleza Rose
Akizingumza kwa kwa lugha ya kabila la Maasai na
kusaidiwa tafsiri na Jirani yake aliyefahamika kwa jina la Samweli ,Rose ameiomba
serikali impatie msaada kwani hapo alipo
ni mlemavu na hakuna chochote ambacho anaweza kufanya cha kumpa rizki.
“Mimi ni miongoni mwa watu ambao nilienda kutembelea
Msomera maisha ya kule nayaona ni mazuri yatanifaa zaidi na nitakuwa
nimesaidiwa sana na serikali, naiomba serikali iharakishe kukamilisha mpango wa
sisi kwenda kule Msomera maana naona kama vile nacheleweshwa kuondoka maana
tunaelendelea kuishi katika mazingira hatari huku hifadhini na wanyama,”
Samweli na Petro Kashuu ni majirani wa mama huyu hapa
wanaeleza namna ambavyo walishuhudia tukio hilo wakisema maisha ya watu katika
eneo hilo yapo hatarini kutokana na uwepo wa Wanyama hatari kama Simba,fisi ,Mbwa
mwitu ,Nyati na Tembo na watu wamekuwa wakiishi kwa hofu.
“Huyu mama wakati alipojeruhiwa na fisi tulikuwepo, na
hili eneo limekuwa na fisi wengi, tumekuwa tukiteswa na Wanyama hapa kijijini,
maisha ya huku ni hatari kwasababu wanyama wamekuwa wakitujeruhi licha ya
kwamba huku watu wamezoea kuishi na Wanyama.
“Yule Fisi baada ya kumshambulia huyu mama alienda
kwenye zizi na kushambulia Ng’ombe wanne ,mmoja alikufa siku hiyo hiyo
akachinjwa watu wakala,baada ya siku mbili wale Ng’ombe wengine walikufa pia “
alisema Kashuu .
Kashuu alisema yule Fisi walifanikiwa kumuua na baadae
alifanyiwa vipimo kwenye kituo cha utafiti na kubainika kw amba alikuwa na
Kichaa cha Mbwa .” Inasemekana yule fisi kabla ya kuja kuvamia kwa huyu mama
aling’atwa na Mbwa akapata kichaa cha Mbwa “.
Naibu Kamishna
Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Elibariki Bajuta amethibitisha
kutokea kwa matukio ya namna hiyo akieleza baada ya tukio la Rose Kapande amesema serikali ilifanya
jitihada za haraka kuokoa maisha ya mwanamke huyo kwa kuhakikisha anapata
matibabu yanayostahili.
“Ni kweli tunafahamu tukio hili la huyu mama kujeruhiwa
na fisi na viungo vyake kuliwa na fisi, huyu mama alikwenda kuokoa mifugo yake
baada ya kusikia fisi ameingia kwenye boma la ng’ombe hivyo wakati anapambana
kuokoa mifugo yake alivamiwa na fisi,”
“Fisi walitafuna viganja vyake vya mikono
na sehemu kubwa ya uso na upande
wa kulia wa kichwa chake na kumuathiri upande wa kulia wa fuvu na sehemu ya
mdomo,”
“Mamlaka kwa kuwa tuna kituo cha ulinzi na timu za
uokoaji baada ya kupata taarifa hizi vijana wetu kwa kushirikiana na majirani
tumlimsaidia kuhakikiasha anapata huduma stahiki,”
Aidha alisema matukio ya watu kuathiriwa na kuvamiwa na
wanyama wakali katika hifadhi hiyo ni mengi
na kwamba yapo matukio ya watu
kuumizwa na wanyama kama vile chui, fisi, simba na tembo .
“Sisi kama Mamlaka tunaendelea kuwaelimisha wananchi
kuchukua tahadhari lakini mnyama ni
mnyama tu hazoeleki, tunafurahi mama huyu kwa sasa anataka kuhama hifadhini
kwenda sehemu anayotaka na suala hili la watu kutakiwa kuhama kwa hiari ni kwa
ajili ya usalama wa maisha yao na uhifadhi.
Mwisho
Comments
Post a Comment