JK AMFAGILIA MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA MOSHI JAFARY MICHAEL.
Rais Jakaya Kikwete akimueleza neno Mstahiki Meya wa manispaa ya Moshi ,Jafary Michael wakati wa sherehe ya ufunguzi wa jengo jipya la Kisasa la Kitega Uchumi la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF. |
Rais Kikwete akizungumza na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Jafary Michael wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la kisasa la NSSF. |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Jakaya Kikwete amepongeza
baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa usimamizi
mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiahidi serikali
kuendelea kutoa pesa kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali.
Mbali na pongezi hizo Rais kikwete pia amebariki jitihada za
halmashauri ya Manispaa ya Moshi za kutaka kubadilika kutoka kuwa
Manispaa na hatimaye kufikia kuwa jiji kama ilivyo jiwekea katika
malengo yake ifikapo mwaka 2015.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la
kisasa la kitega uchumi la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) lililo
gharimu kiasi cha sh Bil, 64 lililojengwa katikati ya mji wa Moshi
ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara mkoani kilimanjaro.
“Mambo mengi mazuri yanaendelea katika mkoa huu(Kilimanjaro )
niendelee kuwapongeza watendaji wengine wa serikali kwa kutekeleza
ilani ya Chama cha Mapinduzi,..hata Mstahiki Meya (Jafary) nakupongeza
tu kwa sababu nyie hamna serikali siye ndio wenye serikali ,kwa hiyo
tunakushukuruni kwa usimamizi wenu mzuri na tutaendelea kuwapeni pesa
kutokana na usimamizi wenu mzuri”alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alimtaka Mstahiki Meya Jafary kuwa Meya wa Maendele kwa
kutengeneza mazingira ya upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa
viwanda pamoja na majengo mbalimbali ambayo yatavutia wawekezaji
zaidi.
“Mkuu wa mkoa ameomba taasisi nyingine zije ,ushauri wangu tu ni
tengeni maeneo ,taasisi hizi zinatafuta maeneo ya kujenga ,hakuna
mahali tutapata? ,lazima Mstahiki Meya uwe meya wa maendeleo .hayo
ndiyo maendeleo yenyewe lazima utenge maeneo mkisha fanya hivyo watu
watakuja lazima mlifikirie hilo” alisema Kikwete ,
Alisema kutokana na ujenzi wa jengo hilo jipya Moshi sasa inaweza
kupokea mikutano mikubwa na kwamba ujenzi huo ni ukombozi kwa
wafanyabiashara mbalimbali wa Manispaa ya Moshi na wale wanaotaka kuja
kufanya shughuli za kibiashara katika mji wa Moshi.
Rais Kikiwete alisema uongozi sio kujisifu na kujisifia tu bali ni
kutenda vitendo na kufanya maamuzi yanayothibisha na yanayolingana na
sifa hizo huku akisifia maono ya maamuzi ya NSSF kwa kuthibitisha kwa
vitendo sifa ambazo shirika hilo linazo.
Awali akizungumza katika shughuli hiyo iliyo iliyohudhuliwa na mamia
ya wananchi na viongozi wa taasisi zilizoko ubia wa ujenzi wa jengo
hilo,Waziri wa Kazi na Ajira ,Gaudensia Kabaka alisema ni muhimu kwa
NSSF kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati na inayolipa badala
ya fedha hizo kubakia kwenye mabenki tu ambako zinaweza kukumbwa na
athari za mfumuko wa bei.
Jengo hilo linalojulikana kama Kilimanjaro Commercial Complex
limejengwa kwa ubia wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii la NSSF
,Taasisi ya Girl Guide Tanzania ,Taasisi ya Red Cross na Chama cha
Uzazi na Malezi Bora Tanzania(UMATI) likiwa ndio jengo kubwa kuliko
yote katika manispaa ya moshi.
Ujenzi wa jengo hilo ambao ulianza Desemba 2011 na kuchukua takribani
miaka mitatu limejengwa kwa pamoja na kampuni ya Group Six
International ya China na Advent Construction ya nchini na litakuwa na
maduka makubwa na madogo ,Maofisi ,Mabenki ,na Kumbi za Mikutano .
Comments
Post a Comment