NJIA YA MBIO ZA KILIMANJARO MARATHON ZAPIMWA NA KURIDHIWA



NJIA mpya zitakazotumika wakati wa mbio za kimataifa za Kilimanjaro mwaka huu, (Kilimanjaro Marathon 2014), zimepimwa na kuridhiwa ambapo mabadiliko hayo yameboreshwa ikilinganishwa na njia za zamani.

 Kwa mujibu wa waandaji, marekebisho hayo yamelenga kuboresha usalama barabarani na kuondoa msongamano wa magari wakati yanaendelea.

Njia zilipimwa na kuridhiwa na katibu wa chama cha kimataifa cha mbio ndefu, (AIMS), Hugh Jones akisaidiana na Michael Hughes wa Nairobi Marathon, Ibrahim Hussein wa shirikisho la vyama vya riadha vya kimataifa, (IAAF), pamoja na John Bayo wa Kilimanjaro Marathon Club.

 Akitoa maoni yake kuhusu njia hizo mpya Jones, alisema “Njia hizi mpya ni nzuri na za kuvutia. Hapa utaona kuwa baada ya kuanza kwa nusu marathon na kuingia nusu ya pili ya mbio hizi kwa ujumla, washiriki watajikuta wakijitahidi kupanda kilima. 

Hii ni sehemu ngumu yenye kuchosha lakini washiriki watakutana na mashabiki wengi watakaokuwa wakiwashangilia na kuwatia moyo. Wakiachana na mashabiki mbele watakutana na mazingira mazuri yenye mashamba ya kahawa, mandhari ya kijani chenye kuvutia na mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro.”

Aliongeza, "Punde watakapoiacha barabara kuu ya lami, washiriki watalazimika kuvuka bonde, kisha kuendelea na mteremko kwenye msitu wa kuvutia kabla ya kurudi tena kwenye barabara ya lami na kuendelea na mbio hizo kwa kilomita 11.5.

 Hatua hii ina mteremko mzuri ambapo safari hii pamoja na kwamba mlima Kilimanjaro utakuwa nyuma ya washiriki lakini mandhari mbele yao bado zitakuwa ni za kuvutia. Wakati wakirudi maeneo ya Moshi Mjini, washiriki watapita chini ya uvuli mzuri wa miti iliyooteshwa kando kando mwa barabara wakati huo watakuwa wakikaribia kumaliza mbio hizo.
 
 Uwanja wa Ushirika ambapo ndicho kituo cha kumalizia umekuwa ni sehemu ya faraja kubwa kwa wakimbiaji ambao huwa wamechoka sana na wakati watakapokuwa wanavuka mstari wa kumalizia na kugeuka nyuma, kwa mbali macho yao yatakutana na mandhari ya kuvutia ya mlima Kilimanjaro, mandhari ambayo itawakumbusha kuwa ndiyo kielelezo kikubwa cha wao kushiriki mbio hizo”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wild Frontiers, John Addison, alisema kuwa njia hizo mpya zilizodhibitishwa hivi karibuni zitakuwa maarufu kutokana na njia hizo kupitia kwenye sehemu ya misitu na mashamba ya kuvutia.

Addison ameendelea kusema kuwa njia hizo mpya zitaboresha usalama barabarani wakati wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Machi 2, 2014 na kwamba zitawapa washiriki faraja na uhakika wa kukimbia kwa uhuru na usalama zaidi.

Alisema mbio za kilomita 42.2 zinatarajiwa kuanza saa 12.30 asubuhi katika uwanja wa Ushirika, (MUCCoBS), wakati zile za kilomita 21 zinatarajwa kuanza saa 1.00 ya asubuhi kuanzia lango kuu la kuingilia chuo cha Ushirika, (MUCCoBS), ulioko barabara ya Sokoine.

Amesema zile za kilomita 10 zitakazowashirikisha watu wenye ulemavu zinazodhaminiwa na Gapco, zinatarajiwa kuanza saa 12.45 asubuhi uwanja wa Ushirika, ambapo zitawashirikisha wale wenye baiskeli za magurudumu na zile zenye kuendeshwa kwa mikono pekee.

Mbio za kujifurahisha za kilomita 5 na ambazo hudhaminiwa na Vodacom, alisema zinatarajiwa kuanza saa 1.45 asubuhi na zitaanzia katika mzunguko wa barabara ulioko karibu na kituo cha YMCA. Mbio zote zinatarajiwa kuishia katika uwanja wa Ushirika, Moshi.

Mbio hizo zimeratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions kama waratibu wa ndani kwa ushirikiano na chama cha riadha nchini, ( AT), chama cha riadha mkoani Kilimanjaro, (KAA), pamoja na Kilimanjaro marathon Club.

Aidha mbio hizo zimedhaminiwa na kufadhiliwa na Kilimanjaro Premium Lager, Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement na KK Security.

 Wengine ni pamoja na Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, kampuni ya magari ya CMC, Rwandair, FNB Tanzania, UNFPA na maji ya Kilimanjaro.

Comments

Popular posts from this blog

MGOMO WA WAFANYABIASHARA WATIKISA MKOANI KILIMANJARO.

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO,SAID MECKY SADICKY AFANYA ZIARA KATIKA MAGHALA NA MADUKA YA MARENGA INVESTMENT KUJIONEA HALI YA TATIZO LA SUKARI

MREMA AENDELEA NA MIKUTANO JIMBONI KWAKE VUNJO