Tizama :MAAJABU YA KILIMANJARO MARATHON MWAKA 2014.



John Bayo akitambulisha wanariadha.

Wanariadha mashuhuri wa Tanzania watapambana vikali ili kushinda medali na fedha katika mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 zinazotarajiwa kufanyika tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.

Mkurugenzi wa Mashindano hayo John Bayo alisema jana kwamba wanariadha maarufu wa Tanzania, Andrew Sambu, John Leonard na Daudi Joseph, ni kati ya wanariadha Watanzania watakaoshiriki katika mbio za kilomita 42 kwa wanaume.

Katika mbio za kilomita 42 kwa wanawake watakuwepo Banuelia Brighton, Fabiola William na Flora Yuda ambao wanatarajia  kutoa upinzani mkali kwa wanariadha wengine Watanzania pamoja na wa kigeni.

Andrew Sambu ana rekodi ya kumaliza Korea Marathon kwa muda wa dakika 2:09:52 mwaka 2004 na mshindi wa medali ya fedha kwenye Mashindano ya Riadha barani Afrika na ameshiriki Olimpiki wakati Banuelia Brighton akiwa ameshinda Kigali Peace Marathon mwaka 2009 na kumaliza wa pili Kampala Marathon mwaka 2011.  

Dickson Marwa mshindi wa Ngorongoro Half marathon 2013
Dickson Marwa – mshindi wa Ngorongoro Half Marathon 2013 ambapo alimaliza na 1:4:49 na Alphonce Felix pamoja na Ezekiel Jafari ni  kati ya wanariadha ambao wataiwakilisha Tanzania kwenye kwenye mbio za kilomita 21 kwa wanaume huku upande wa wanawake ukitarajia kuwakilishwa na Mary Naali, Jacqueline Sakilu na Sarah Ramadhani.

Akiwa ametengeneza rekodi nyingi, Mary Naali ni kati ya wanariadha bora nchini katika mbio za kilomita 21 maarufu kama Half Marathon. 

Alishinda Vienna Marathon mwaka 2010 ambapo alimaliza katika muda wa 1:12:16 na baada ya hapo akavunja rekodi kwenye mbio za kilomita 25 za Arusha VIP Race mwaka 2011 ambapo alishinda kwa 1 1:20:52 na kuvunja rekodi ya 1:22:18 iliyokuwa imewekwa na Josephine Deemay mwaka 2006. Mei mwaka 2013 pia alishinda mbio ya Bucharest International Marathonihuko Romania akimaliza katika muda wa 1:16:32.

Naali atashindana na Sarah Ramadhani ambaye ni bingwa mtetezi kutokana na ushindi wake kwenye 2013 Kilimanjaro Marathon ambapo alimaliza mbio akiwa na 1:13:05. Pia katika mpambano huo atakuwemo Jacqueline Sakilu ambaye ni kati ya wanariadha wanaotarajiwa kufanya makubwa baada ya kushinda mbio kadhaa za kilomita 21 ikiwemo Uhuru Marathon (1:15:25) na Ngorongoro Run kwa 1:16:50.

 “Tuna furaha kuwa na kikosi madhubuti kwa wanaume na wanawake,” alisema John Bayo ambaye pia ni kocha maarufu wa riadha. “Uwepo wa wanariadha hawa wazoefu naamini utaifanya mbio hii iwe ya kuvutia.”

“Wanariadha wetu wana viwango vya kimataifa. Baadhi ya wanairiadha wa kiume wameishakimbia chini ya muda wa masaa 2:15:00 huku upande wa wanawake wakiwa wamekimbia chini ya 2:40:00.Hii ni mbio ya kimataifa ambapo mshindi anaweza kuwa mtu yoyote kutoka taifa lolote lakini kinachotupa nguvu ni hamasa tunayoipata kutoka kwa wananchi maana mbio inafanyika hapa nyumbani, hivyo basi tuko tayari kwa changamoto hii,” alisema.

Aggrey Mareale mkurugenzi mkuu Executive Solutions.
Nae Aggrey Marealle Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo amethibitisha kwamba timu ya wanariadha inayoandaliwa na Holili Athletics Club imekuwa katika maandalizi kwa miezi 8 iliyopita na wako tayari kupeperusha bendera. 

Timu hiyo imepunguzwa kutoka wanariadha 20 hadi 8 bora ambao wako kwenye maandalizi ya mwisho. Wanariadha wa kambi hiyo wameonyesha mafanikio baada ya kushinda Rock City Marathon na Dar Rotary Marathon.

John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo amesema takribani washiriki 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 kutoka mabara sita wanatarajiwa kushiriki kwenye mbio za 12 za Kilimanjaro Marathon.

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2014 zinaratibiwa na Executive Solutions kwa ushirikiano na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club. Mbio hizo zinadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager (wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement,KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.

Comments

  1. Tunangojea hiyo siku kwa hamu kubwa hasa sie wakazi wa Moshi.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

MGOMO WA WAFANYABIASHARA WATIKISA MKOANI KILIMANJARO.

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO,SAID MECKY SADICKY AFANYA ZIARA KATIKA MAGHALA NA MADUKA YA MARENGA INVESTMENT KUJIONEA HALI YA TATIZO LA SUKARI

MAKATIBU WA CCM VUNJO WASEMA HAWANA UGOMVI NA KATIBU WAO WA WILAYA.