TANAPA YATAJA MAJINA 10 YA WANAHABARI WATAKAO WANIA TUZO .
![]() | |
Meneja uhusiano wa mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA),Paschal Shelutete akizungumza wanahabari kuhusiana na tuzo za Uandishi wa Habari za Shirika la Hifadhi za Taifa za mwaka 2013. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAANDISHI 10 WAFIKA FAINALI TUZO ZA HABARI ZA TANAPA ZA 2013.
WAANDISHI 10 WAFIKA FAINALI TUZO ZA HABARI ZA TANAPA ZA 2013.
Jumla ya Waandishi wa Habari 10 wamefanikiwa kufikia hatua ya fainali ya Tuzo za Uandishi wa Habari za Shirika la Hifadhi za Taifa za mwaka 2013.
Wanahabari waliofanikiwa kufika hatua ya fainali ni
pamoja na Frank Leonard (Habari Leo), Jackson Kalindimya (Nipashe), Humphrey
Mgonja (Radio SAUT FM), Raymond Nyamwihula (Star TV) na Vedasto Msungu (ITV).
Wengine ni pamoja na Kakuru Msimu (Star TV), Gerald
Kitabu (The Guardian), Salome Kitomari (Nipashe), David Rwenyagira (Radio 5) na
Cassius Mdami (Channel Ten).
Hafla ya utoaji Tuzo za Habari za TANAPA itafanyika
siku ya Jumanne tarehe 27 Mei, 2014 jijini Mwanza ambapo Mgeni Rasmi
anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu.
Hafla hii itaenda pamoja na Mkutano wa kila mwaka
baina ya TANAPA na Wahariri wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari
nchini inayotarajiwa kuanza wiki ijayo jijini Mwanza.
Jumla ya kazi zilizotumwa kwa ajili ya
kushindanishwa mwaka huu ni 114 tofauti na kazi 34 za mwaka jana. Ongezeko hili
la asilimia 235 lililazimu Jopo la Majaji kutumia muda mwingi zaidi wa kupitia
kazi zote na kupata washindi. Kati ya kazi 114 zilizotumwa, kazi zilizohusu
Uhifadhi ni 64 (sawa na 56%) na kazi zilizohusu Utalii wa Ndani zilikuwa 50
(sawa na 44%).
Tuzo za Uandishi wa Habari za TANAPA hutolewa kila
mwaka kwa nia ya kuwashirikisha wanahabari kushindanisha umahiri wa kazi zao
katika kuelimisha jamii umuhimu wa dhana ya Uhifadhi kwa maeneo yaliyotengwa
kisheria kama Hifadhi za Taifa na uhamasishaji wa Utalii wa Ndani kwa faida ya
uchumi wa nchi yetu.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
23.05.2014
Hifadhi za Taifa Tanzania
23.05.2014
Comments
Post a Comment