NYALANDU KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UTALII NCHINI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, ameendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu kuhusiana na
changamoto zinazowakumba wadau wa biashara ya utalii nchini.
Katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa mafanikio na kwa haraka, Nyalandu ametangaza
kuanza kwa vikao vitakavyowakutanisha wataalamu wa Wizara zinazohusika na
maliasili na utalii za Tanzania na Kenya kwa lengo la kujadiliana masuala
mbalimbali iili yapatiwe ufumbuzi kwa maslahi ya pande zote.
Hatua hiyo imetokana na hivi karibuni Serikali ya Kenya kuyazuia magari ya
utalii kutoka Tanzania kuingiza watalii kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Jomo Kenyatta, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.
Hata hivyo, Nyalandu aliingilia kati kwa kuzungumza na Waziri wa Utalii wa
Kenya, Phillys Kandie na kufikiwa kwa makubaliano ya kuruhusiwa na hapo wazo wa
wizara hizo kukutana likaibuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Nyalandu alisema vikao
ya wataalamu hao vitaanza rasmi Februari 3, mwaka huu, jijini Arusha ambapo vitahusisha
pia wataalamu kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Alisema vikao hivyo vitajadili masuala mbalimbali ili kuhakikisha changamoto
zote zinawaikabili sekta ya utalii kwa nchi hizo mbili zinapatiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuimarisha ushirikiano pamoja na
kuongeza ulinzi kwenye mbuga za wanyama na mapori ya akiba dhidi ya mtandao wa
ujangili.
Hata hivyo, aliweka wazi kuwa hoja kuhusiana na mpaka wa Borongoja
haitajadiliwa kwenye vikao hivyo kwa kuwa si sehemu ya ajenda.
“Nchi zetu hizi zinategemeana sana katika biashara ya utalii hivyo, kuna
makubaliano tuliyafikia muda mrefu huko nyuma lakini yanaonekana kuanza kuwa na
changamoto hivyo ni lazima tujadili ili tuweze kusonga mbele. Hatutaki watalii
wanaokuja kupumzika wasumbuke kwani itakuwa ni hasara kwa wafanyabiashara wetu
na kutahatarisha uchumi wa taifa…daima lazima tusonge mbele,” alisema Nyalandu.
Aliongeza kuwa baada ya mkutano wa wataalamu utafuatiwa na wa makatibu wakuu wa
wizara hizo utakaofanyika Februari 4 mwaka huu kisha utahitimishwa na wa
mawaziri utakaofanyika Februari 5.
Nyalandu alisema ana imani mikutano hiyo itatoka na mwanga mpya na maboresho
kwa sekta ya utalii na kusisitiza maslahi ya pande zote yatazingatiwa.
Alisema kuwa nia ya Tanzania ni kuendeleza Jumuia ya Afrika Mashariki na
mahusiano yake mazuri na si kugombana na kuharibu uhusiano huo.
Alisema daima Tanzania itakuwa makini kuhakikisha mahusiano yanakaa sawa katika
majadiliano hayo na kwamba kusije kutokea jambo likaleta madhara kwa watu
wengine.
Nyalandu aliongeza Tanzania itafanya biashara za utalii na watu wengine
kuhakikisha wanaendelea kulinda rasilimali za taifa sambamba na wafanyabiashara
wakubwa wa kitalii na wadogo
Comments
Post a Comment