HUDUMA YA UOKOAJI KWA KUTUMIA HELIKOPTA YAANZISHWA MLIMA KILIMANJARO.

Moja ya ndege aina ya Helkopta ilipowasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya utoaji wa Huduma ya Utafutaji na uokoaji kwa wapanda Milima
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kilimanjaro SAR ya mkoani Kilimanjaro Ivan Broun akionekana mwenye tabasamu mara baada ya moja ya ndege aina ya Helkopta kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya utoaji wa Huduma ya Utafutaji na uokoaji kwa wapanda Milima.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini .

KAMPUNI ya Kilimanjaro SAR ya mkoani Kilimanjaro imeanza rasmi shughuli za utafutaji na uokoaji kwa wapandaji wa Milima miwili ya Kilimanjaro na Meru kwa kutumia ndege aina ya Helkopta.

Kilimanjaro SAR inakua kampuni ya kwanza kuweka historia katika bara la Afrika ya utoaji wa huduma hiyo  muhimu na maada kwa maisha ya wapandaji wa Milima ikizingatiwa asilimia 75 ya magonjwa uwapo mlimani yanatokana na mbadiliko ya Hali ya Hewa kulingana na urefu wa Mlima.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Afisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Kilimanjaro SAR,Ivan Braun raia wa Denmark ameeleza kuwa kuanza kwa shughuli  hiyo kutasaidia aliyepata matatizo akiwa mlimani kuhudumiwa ndani ya dakika 5 baada ya kupokea simu ya hitaji la msaada.

“Kampuni hii itatoa huduma kamili ya uokoaji wa dharura kwa wapanda Mlima,Takwimu zinaonyesha zaidi ya watalii 45,000 hutamani kupanda kilele cha mlima mrefu Africa, kwa bahati mbaya hofu juu ya usalama wa maisha yao imekua kizuizi kwao kutimiza ndoto hii.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

“Mabadiliko chanya sasa yamepatikana kutoka katika huduma za uokoaji zisizo na ufanisi mpaka zenye ubora wa hali ya juu.”alieleza Braun ambaye ni mtaalamu wa kupanda Milima.

Alisema mbali na kuwa na Helikopta bora na zenye uwezo wa juu maalumu kwa huduma hiyo  ya utafutaji na uokoaji pia ina timu maalumu ya madaktari wa kimataifa na wasaidizi wa kliniki.

“Kampuni hii inaleta usalama katika maana pana zaidi kwa kuanzisha kliniki ya kwanza Afrika maalumu kwa matibabu ya magonjwa yatokanayo na mlima.Kampuni ya Kilimanjaro SAR itahakikisha inaifanya Kilimanjaro kuwa sehemu salama zaidi ya utalii Africa.”alisema Braun.

Kuanza kwa utolewaji wa huduma hiyo kutasaidia sekta ya Utalii nchini kupata suluhu ya Changamoto ya muda mrefu ya utoaji wa msaada wa kitabibu, utafutaji na uokoaji wa wageni wanaopata matatizo wakati wa kupanda Mlima Kilimanjaro na Meru .

Hivi karibuni kampuni ya Kilimanjaro SAR iliingia makubaliano na Hospitali ya St Joseph ya mjini Moshi kuanza kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa watakao pata matatizo wakati wa kupanda Milima hiyo zoezi lililoenda sambamba na uzinduzi wa Kliniki ya kwanza Afrika ya magonjwa yatokanayo na muinuko wa juu.

Katika uzinduzi huo mgeni rasmi ,Mkuu wa wilaya ya Moshi ,Kippi Warioba alisema hii ni fursa mpya kwa sekta ya Utalii kuutangaza vyema Mlima Kilimanjaro kwamba kwa kiasi kikubwa itasaidia katika kuongeza idadi ya Watalii. 

Hata hivyo kuanza kwa huduma hiyo muhimu kwa sekta ya Utalii nchini ,bado ipo changamoto ya matumizi ya uwanja mdogo wa ndege wa Moshi hali inayowalazimu kutumia uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).

Mwisho









Comments

Popular posts from this blog

MAKATIBU WA CCM VUNJO WASEMA HAWANA UGOMVI NA KATIBU WAO WA WILAYA.

TIB YAKABIDHI MICHORO HALISI YA KITUO CHA MABASI KWA UONGOZI WA MANISPAA YA MOSHI.

BENKI KUU YATOA TAARIFA KUHUSU UPOTOSHAJI JUU YA SARAFU YA SH ,500/