EFTA KUONGEZA IDADI YA WATUMIAJI WA TREKTA
Afisa Uendeshaji Mkuu wa EFTA (aliyekaa) Bwana Leonce Malamsha akimsajili mmoja wa washiriki waliohuduria mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima wa Kilombero, yaliyokuwa yameandaliwa na taasisi ya EFTA
Morogoro
TAASISI inayojihusisha na utoaji wa mikopo ya mashine kwa wakulima ya EFTA imejipanga kuongeza idadi ya wakulima wanaomiliki matrekta hapa nchini lengo likiwa ni kuchochea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa wingi .
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya EFTA, Bw,Nicomed Bohay ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima wa Mkoa Morogoro, mafunzo yaliyofanyika katika mamlaka ya mji wa Ifakara yakiwa na lengo la kuwafundisha wakulima umuhimu wa kilimo cha kisasa.
Alisema katika kufanikisha adhma hiyo EFTA ikishirikiana na kampuni ya Kilimo ya Hughes ya jijini Arusha wameandaa mkakati wa kutoa mikopo ya matrekta aina ya New Holland TT75 zaidi ya mia mbili kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro pamoja na maeneo mengine nchini .
“Tunataka kupanua wigo wa idadi ya wakulima wanaomiliki matrekta hapa nchi, na ndio maana tumewaletea wakulima hawa mikopo ya matrekta kwa wingi, na tunaamini hatua hii itachochea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa wingi na hivyo kuwaongezea tija,” amesema Bohay
Bohay alisema wakulima wanategemea kunufaika na fursa ya mikopo ya matrekta pamoja na vipuri vyake,mikopo ambayo itakuwa na masharti nafuu na itapatikana kwa kila mkulima nchini bila dhamana yoyote.
“Mikopo hii tunayoileta kwa wakulima haina dhamana, isipokuwa trekta litakalokopwa ndio litakuwa dhamana yenyewe, hivyo wakulima msiogope kukopa maana hatutahitaji nyumba wala mali yako yoyote, Lengo letu sisi ni kuwawezesha wakulima nchini kubadilika kutoka kilimo chamazoea na kuwa wakulima wa kisasa kwa kumiliki na kutumia zana bora za kilimo” aliongeza Bohay.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya aliwataka wakulima katika wilaya ya Kilombero kuchangamkia fursa hiyo, ambayo imekuja kuchochea juhudi za serikali za kumkomboa mkulima wa Tanzania kutoka katika kilimo cha mazoea na Kwenda katika Kilimo cha Kisasa.
“Tumelima kilimo cha mazoea kwa muda sasa nadhani sasa ni wakati wa kubadilika na kuwa na mitazamo ya kisasa ambayo itatuletea tija katika shughuli zetu”alisema Kyoba.
Alisema Kilombero kuna wakulima na wafugaji wengi ambao bado wanalima kwa mazoea na hawa kwa sehemu kubwa ndio wamekuwa sehemu ya wale wanaochangia katika uhalibifu wa mazingira yetu.
“Kama serikali tumetoa maelekezo kwa makundi yote, wakulima pamoja na wafugaji kusitisha mara moja shughuli zao katika maeneo ya vyanzo vya maji na Pori la Akiba la Kilombero tunataka maeneo haya yalindwe na kila mmoja wetu maana yanatusaidia wote katika shughuli zetu za kilimo” alisema Kyoba.
“Wakati tukianza kufuata maelekezo ya serikali, tuchukue sasa na elimu tuliyoipata hapa ili ikatusaidie kubadilisha mtazamo wetu katika kilimo ili tulime kisasa na kupata mafanikio Zaidi” aliongeza Kyoba.
Wilaya ya Kilombero ina ukubwa wa mita za mraba 14,958, vitongoji 458, vijiji 110, mitaa 55, kata 35 na tarafa 5, na inasifika sana kwa kilimo na hususani kilimo cha Miwa na Mpunga.
Mwisho.
Comments
Post a Comment