MWISHAWA NAIBU KAMISHNA MPYA TANAPA
ARUSHA
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Nassoro Kuji ameongoza
uapisho wa Naibu Kamishna mpya wa Uhifadhi Massana Gibril Mwishawa
anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara katika Shirika la Hifadhi za
Tanzania (TANAPA).
Hafla ya uapisho iliyofanyika Makao Makuu ya TANAPA jijini, Arusha imeambatana na uvishwaji wa
cheo kipya cha Naibu Kamishna wa Uhifadhi ambapo katika salamu za Pongezi Kamishna wa
Uhifadhi TANAPA Musa Kuji amesisitiza uwajibikaji na kumtanguliza Mungu katika
kutekeleza majukumu hayo ya Naibu Kamishna wa Uhifadhi.
”Cheo huambatana na
majukumu na uwajibikaji. Hivyo basi, ni muhimu ukamtanguliza Mwenyezi Mungu
wakati wote ili aweze kukuongoza katika utekelezaji wa majukumu yako haya
mapya. Taaluma, uzoefu, umahiri na kujituma kwako, kunatupatia imani kubwa kuwa
utatekeleza majukumu yako kwa uadilifu, weledi, bidii kubwa na bila woga wala
upendeleo” alisisitiza Kamishna Kuji
Aidha, Kamishna Kuji
aliongeza kuwa katika nafasi ya Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia
Maendeleo ya Biashara kipaumbele cha kwanza cha Shirika ni usalama wa
rasilimali za Taifa na utolewaji wa huduma bora kwa wateja wakiwemo Watalii na
kusisitiza zaidi ubunifu katika mikakati endelevu katika kuinua utalii na
Uhifadhi.
Naye, Naibu Kamishna
wa Uhifadhi Massana Gibril Mwishawa ameishukuru Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kwa
kumteua kushika nafasi hiyo ya Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya
Biashara lakini pia Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa jitihada zake za makusudi anazoendelea kuzifanya katika kuinua
sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini.
“Mmenipa deni kubwa sana kwenu kwa watumishi wote nitakao
waongoza natambua cheo nilichovishwa leo kina majukumu makubwa ambayo
yananihitaji kuwajibika kikamilifu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za
kiuhifadhi zilizopo sasa na kuimarisha uhifadhi na utalii ndani ya shirika
ninaahidi nitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Hifadhi zote za
Taifa” alisema Kamishna Mwishawa
Bodi ya Wadhamini ya TANAPA tarehe 29.04.2024 ilimteuwa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Massana Gibril Mwishawa kuwa Naibu Kamishna wa
Uhifadhi anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, awali kabla ya
uteuzi huo alikuwa Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki akisimamia Hifadhi ya
Taifa Nyerere, Mikumi, Saadani, na Milima ya Udzungwa.
Comments
Post a Comment