MAPATO MANISPAA YA MOSHI "YAPAA" KUTOKA BILIONI 6.1 HADI BILIONI 9.9
Na Dixon Hussein - Moshi
Manispaa ya Moshi imepiga hatua kubwa
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, ikiongeza mapato kutoka bilioni 6.1 mwaka
2021 hadi bilioni 9.9 mwaka 2025, ongezeko la takribani bilioni 3.7.
Mafanikio haya yanatajwa kuwa matokeo ya mikakati madhubuti
iliyowekwa ili kuboresha vyanzo vya mapato na kuongeza uwajibikaji katika
usimamizi wa rasilimali za umma.
Akizungumza katika kikao cha bajeti cha mwaka wa fedha
2025/26, Meya wa Manispaa ya Moshi Zuberi Kidumo amesema kuwa ongezeko hilo
limechangiwa na mbinu mpya za ukusanyaji wa mapato pamoja na uwekezaji katika
miradi yenye tija.
"Tumeimarisha mifumo yetu ya ukusanyaji wa mapato kwa
kutumia teknolojia ya kisasa, tumeongeza uwazi katika makusanyo, na pia
tumewekeza katika miradi inayozalisha kipato kwa manispaa. Hatua hizi
zimechangia ongezeko kubwa la mapato," alisema Zuberi Kidumo .
Alisema miongoni mwa mikakati iliyochangia ongezeko la
mapato ni matumizi ya Mfumo wa Kidigitali katika Ukusanyaji wa Mapato na kwamba
mifumo hiyo imepunguza upotevu wa mapato
na kuongeza uwazi.
“Mfumo huu umesaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato
yanayotokana na malipo ya moja kwa moja bila kufuata taratibu sahihi” alisema
Kidumo
Akiwasilisha hoja kwa wajumbe wa baraza la Halmashauri ya Manispaa
ya Moshi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe amesema ofisi
yake kwa sasa imewekeza kwenye miradi mitatu ya kimkakatai .
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ni ujenzi wa vibanda
vingi vya biashara katika eneo la Uhuru Park ,Ujenzi wa bustani na kumbi za nje
kwa ajili ya sherehe kwa maharusi pamoja na ukarabati mkubwa wa uwanja wa
michezo wa Majengo .
Mkurugenzi Nasombe anasema Manispaa imeanzisha mfumo wa
ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha kuwa mapato yanayokusanywa yanafika kwenye
mfuko wa manispaa bila upotevu huku usimamizi mzuri wa rasilimali na
uwajibikaji wa watendaji umeimarishwa ili kuhakikisha kila senti inayokusanywa
inatumika kwa maendeleo ya wananchi.
Aidha ameeleza kuwa kumekuwa na ushirikiano mzuri na na taasisi mbalimbali za maendeleo,
wafanyabiashara, na mashirika ya kimataifa katika kutafuta njia bora za
kuongeza mapato na kuwekeza katika miradi mipya.
Mafanikio haya yameifanya Manispaa ya Moshi kuwa mfano wa
kuigwa katika usimamizi wa fedha za umma, huku kukiwa na matumaini makubwa kuwa
mapato yataendelea kuongezeka.
Hata hivyo, changamoto kama ukwepaji wa kodi na uhaba wa
baadhi ya miundombinu bado zinahitaji suluhisho la haraka.
Baadhi ya wananchi wamesifu juhudi za manispaa lakini
wakatoa wito wa uwazi zaidi katika matumizi ya mapato hayo.
"Tunafurahia kuona mapato yanaongezeka, lakini
tunahitaji kuona miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kasi ili wananchi waone
matunda ya mapato haya," alisema mkazi mmoja wa Moshi”.alisema Idrisa Mombo
mkazi wa manispaa ya Moshi
Kwa ongezeko hili la mapato, Manispaa ya Moshi inaonekana
kuwa na dira thabiti ya maendeleo. Swali linalosalia ni je, mapato haya
yataweza kuendelea kuongezeka kwa miaka ijayo na kubadili kabisa taswira ya
kiuchumi ya manispaa?
Mwisho
Comments
Post a Comment