WANAFUNZI TPC WADANDIA “KIBERENGE “CHA MIWA KURUDI MAKWAO ,ABC IMPACT WATOA BAISKELI .












Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari TPC iliyopo wilaya
ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro wanatajwa kuwa katika hali ya kuhatarisha maisha
kutokana na tabia ya kudandia Garimoshi (Treni), maarufu kama Loko wakati wa
kwenda na kurudi shuleni.
Hayo yamebainishwa na baadhi ya wanafunzi pamoja na walimu
wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa
mpango wa kusaidia wanafunzi wa kike wanaosoma shule ambazo ziko mbali
na mahala wanapoishi,mpango unaratibiwa na taasisi ya ABC Impact .
Wanafunzi hao wanadaiwa kutumia treni ambazo zimekua
zikitumika kubeba miwa kutoka mashambani kupeleka kiwandani hatuainayotajwa
kuwa ni hatarishi kwa maisha yao hasa kwa wanafunzi wakike .
Katika jitihada za kuboresha usafiri wa wanafunzi wa kike na
kupunguza changamoto wanazokumbana nazo wakati wa kwenda shule, taasisi ya ABC
Impact imetoa msaada wa baiskeli kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari TPC.
Hii ni sehemu ya mpango wao wa kusaidia wanafunzi
wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni kwa wakati na kuongeza ufanisi wao
katika masomo.
Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa baiskeli hizo,
Mkuu wa Shule ya Sekondari TPC Salehe Shekibwai amesisitiza kuwa msaada huu ni
fursa muhimu kwa wazazi kushiriki katika kuwawezesha watoto wao kupata usafiri
salama.
“ABC Impact wameonyesha moyo wa upendo kwa kugawa baiskeli
hizi, lakini wazazi pia wanapaswa kushiriki kwa kuchangia sehemu ya gharama.
Hili litawafanya wanafunzi kuthamini baiskeli wanazopata,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya ABC Impact Ayanna
Kimaro alieleza kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata usafiri
wa uhakika ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri elimu yao, ikiwa ni
pamoja na kuchelewa kufika shuleni na hatari za barabarani kama kuomba lifti
kwa magari yasiyo salama.
“Tunataka kuona kila
mwanafunzi anapata fursa ya kusoma bila kikwazo cha usafiri. Tunaamini kuwa
kila baiskeli tunayotoa ni mbegu ya mafanikio kwa mtoto wa Kitanzania,”
aliongeza mkurugenzi Ayyana.
Mmoja wa wanafunzi walionufaika na msaada huo Paschal Paul alieleza
furaha yake kwa kupokea baiskeli, akisema itamsaidia kufika shuleni kwa wakati
na kuwa na muda wa kutosha kwa masomo na shughuli nyingine za kielimu.
“Zamani nilikuwa nikichelewa kufika shuleni kutokana na
umbali mrefu, lakini sasa nitakuwa nakuja kwa wakati,” alisema mwanafunzi huyo.
Diwani wa kataya Arusha Chini Leonard Waziri alitoa pongezi kwa Taasisi ya ABC Impact kwa
hatua yao ya kusaidia sekta ya elimu kupitia usafiri.
Alibainisha kuwa wazazi wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo
kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanazitunza baiskeli hizo na kuzitumia kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Pia Waziri alisisitiza umuhimu wa usalama wa barabarani kwa
wanafunzi, akiwataka kutumia baiskeli zao kwa tahadhari kubwa ili kuepuka
ajali.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na walimu, wazazi na viongozi wa
jamii, ambao kwa pamoja walikubaliana kuwa msaada huu utakuwa na manufaa
makubwa kwa elimu ya watoto wa kike na kuwapunguzia mzigo wa kutembea umbali
mrefu kila siku kwenda shuleni.
Mwisho
Comments
Post a Comment